TUICO YAREJESHA TABASAMU LA WAFANYAKAZI 39 WA BIG BON, NEW MSIMBAZI KEROSINE, MSA

 

Tanzania kama ilivyo kwa maeneo mengine duniani, ugonjwa wa Covid-19 umeathiri ulimwengu wa kazi. Waajiri wengi wamefunga biashara au kazi za kwa kuhofia kufa kibiashara. Na hata kwa wale ambao hawafungi biashara zao, basi wanatumia mbinu ya kupunguza wafanyakazi au kutoa likizo kwa wafanyakazi kwa kipindi fulani.


Licha ya kwamba Covid-19 imeleta ugumu kwenye namna ambavyo biashara nyingi zinafanyika. Lakini kuna waajiri wachache wanaotumia mwanya wa janga hili kukiuka haki, heshima na maslahi ya wafanyakazi hali ambayo sio tu kinyume na sheria mbalimbali za kazi ikiwemo ile Sheria ya Ajira na Muhusaino Kazini Na.6 ya Mwaka 2004 bali ni kinyume na utu.

Mathalani, waajiri wa makampuni ya New Msimbazi Kerosine Limited, Big Bon Petroleum Limited  na MSA Transport Company Limited, yote ya Dar es Salaam walitangaza kutoa likizo kwa wafanyakazi 39 pasipo malipo hali iliyosababisha taharuki kwa wafanyakazi hao.

Wafanyakazi wa Big Bon Petroleum katika hafla ya kusaini makubaliano ya mkataba wao wa mapumziko .(Garden Leave).

Lakini Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kwa kushirikiana na vyama vingine vya wafanyakazi, wawakilishi wa wafanyakazi na makampuni ya New Msimbazi Kerosine Limited, Big Bon Petroleum Limited  na MSA Transport Company Limited, yote ya Dar es Salaam imefanikiwa kufikia makubaliano yenye tija kwa wafanyakazi 39 wa makampuni hayo.

Viongozi wa Big Bon Petroleum, Wafanyakazi na Viongozi wa TUICO katika picha ya pamoja baada ya kusaini makubaliano ya mkataba wa garden leave wenye malipo.

Kulingana na makubaliano hayo, wafanyakazi 39 watapewa likizo (garden leave) ya miezi mitatu yenye malipo, iliyoanza Juni Mosi hadi Septemba Mosi, 2020 kwa sababu za kupungua kwa kazi kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa na kusababisha kazi nyingi kusimama.

Katika makubaliano hayo wafanyakazi wanaolipwa mshahara wa shilingi za kitanzania 150,000-180,000 watalipwa shilingi 100,000; wanaolipwa mshahara wa 200,000 hadi 250,000 watalipwa asilimia 50 ya mshahara huku wafanyakazi wanaolipwa mshahara wa shilingi 250,000 na kuendelea watatakiwa kulipwa asilimia 35 ya mshahara wao.

Sambamba na hayo, pia waajiri watawalipia wafanyakazi asilimia kumi ya mchango kwenye mfuko wa hifadhi ya jamiii NSSF kwa kipindi chote cha miezi mitatu watakayochukua likizo kama sheria inavyoelekeza.

Wafanyakazi wa Big Bon Petroleum katika picha moja na viongozi kutoka TUICO Makao Makuu baada ya kusaini mkataba wao wa Garden Leave.

Aidha makubaliano hayo yameeleza kuwa taratibu zingine za ajira zitaendelea kubaki vilevile na endapo hali ya janga la ugonjwa wa Covid-19 itakuwa shwari kabla ya mwezi Septemba mwajiri atatakiwa kuwaita wafanyakazi kurudi kazini, vinginevyo kama hali haitakuwa sio shwari hadi Septemba Mosi, mwajiri atatakiwa kukaa na wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi ili kujadili hatma ya ajira zao.


Related

Recent News 6519433194353105984

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress