Viwanda, Watoaji Wakubwa wa Ajira Kwa Vijana. Je, Vipi Kuhusu Maslahi Yao?

Sekta binafsi ni mwajiri mkubwa wa vijana hapa nchini. Kulingana na utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwenye vipato vya ajira rasmi Tanzania bara mwaka 2016, sekta binafsi inaajiri asilimia 60.1 ya vijana wenye umri kati ya 15-35.

Wafanyakazi wa kiwanda cha uzalishaji wa jezi za mpira cha Mazava kilichopo mkoani Morogoro.

Hii inamaanisha kuwa kati ya vijana 10 wenye umri wa miaka 15-35 nchini, 6 wameajiriwa katika sekta binafsi ukilinganisha na asilimia 40 ya vijana ambao wameajiriwa kwenye sekta za umma.

Utafiti huo unaonesha kuwa viwanda vya uzalishaji vilishika nafasi ya pili kwa asilimia 18.1 ya ajira zote za vijana nchini baada ya sekta ya elimu ambayo imeajiri asilimia 18.5 ya vijana wenye umri wa miaka 15-35.

Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri TUICO, ambacho pia kinasajili wanachama kutoka sekta hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa kuajiri vijana wengi hapa nchini, kinatambua nafasi ya sekta binafsi katika kutatua changamoto ya ajira.

Mathalani, viwanda vya uzalishaji vinaongoza kwa kutoa ajira za muda mfupi ambazo mikataba yake haidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja. Na mara nyingi vijana hawa wanapata ujira kila siku ili kuendesha maisha yao.

Hata hivyo, kundi hili la vijana wanaofanya kazi katika sekta hii ya uzalishaji wanakutana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ujira mdogo, baadhi ya waajiri wakorofi hawapendi vyama vya wafanyakazi sehemu za kazi licha ya kwamba ni haki ya mfanyakazi. Pamoja na uelewa mdogo wa vijana juu ya vyama vya wafanyakazi na umuhimu wake.

Utafiti huo wa NBS ulionesha kuwa waajiri wengi katika sekta binafsi ni wale wa viwanda vya uzalishaji kwa asilimia 26.9 mwaka 2016 ikifuatiwa na biashara za jumla na ndogondogo, mafundi magari na shughuli za huduma za vyakula kwa asilimia 10.2.

Friedrick Mng’ong’o  Mkuu wa Idara ya Elimu, Vijana na Uimarishaji TUICO Makao Makuu

“Tunatambua mchango wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa taifa hasa katika utoaji wa ajira kwa vijana.Tumeendelea kufanya uhamasishaji na kutoa elimu juu ya harakati za vyama vya wafanyakazi na umuhimu wake” Friedrick Mng’ong’o ambaye ni Mkuu wa Idara ya Elimu, Vijana na Uimarishaji TUICO Makao Makuu

Katika  kuhakikisha haki, heshima na masilahi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa vinalindwa, TUICO imeendelea na uhamasishaji juu ya umuhimu wa vyama vya wafanyakazi ambapo uhamasishaji huu umesaidia vijana kuutambua umuhimu wake kujiunga na TUICO.

Wafanyakazi wa kiwanda cha Lodhia Steel Industries Limited cha Dar es Salaam.

Kwa kipindi cha mwezi huu wa Julai 2020, TUICO imesajili zaidi ya vijana 100 kutoka Lodhia Steel Industries Limited. Aidha, chama kimeendelea kukaa na waajiri kwa majadiliano ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi hao kupitia mikataba ya hali bora za kazi.


Related

Youth 2960382339696817243

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress