Wafanyakazi 246 Wajiunga na TUICO Mradi wa Umeme Mto Rufiji

Wafanyakazi takribani 246 ndani ya eneo
la Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Uzalishaji Umeme katika Maporomoko ya Mto Rufiji
[Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP)] mkoani Pwani wamejiunga na Chama
cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).
![]() |
Mkuu wa Sekta ya Biashara TUICO, Ndugu Peles Jonathan akizungumza na wafanyakazi katika eneo la Mradi wa Umeme wa Nyerere, Mto Rufiji, Mkoani Pwani. Julai 2020. |
Hatua hii inafuatia kambi ya siku tano iliyofanywa na timu kutoka TUICO Makao Makuu Dar es Salaam kwenye eneo hilo ambapo waliwahamasisha wafanyakazi ndani ya mradi wa JNHPP kujiunga na TUICO kutokana na umuhimu wake katika utetezi wa haki na maslahi yao; afya na usalama mahala pa kazi, sambamba na elimu nyingine muhimu ambazo TUICO imekuwa ikitoa kwa wafanyakazi hapa nchini.
Mbali na hatua hiyo, TUICO imefanikiwa kuunda matawi mapya mawili sambamba na zoezi la uchaguzi katika matawi saba ndani ya JNHPP na kupata viongozi wapya ambao watawaongoza wafanyakazi wenzao ambao
ni wanachama wa TUICO katika eneo hilo la kimkakati kwa kipindi cha miaka mitano.
Kukamilika kwa mradi huo wa JNHP kutapelekea uzalishaji wa kiasi cha Megawati 2,115 za
umeme ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuifanya Tanzania kuwa na
umeme mwingi na wa uhakika.