Hakuna Mafanikio ya Maana Anayoweza Kupata Mfanyakazi Peke Yake Katika Kupigania Haki Yake

Vyama vya wafanyakazi ni asasi muhimu katika ulimwengu wa kazi. Vyama vya wafanyakazi ni daraja baina ya tabaka la wafanyakazi, waajiri na serikali. Kwa sababu malengo ya wafanyakazi na waajiri hayakubaliani, migogoro baina ya tabaka mbili hizi ni vitu vinavyotarajiwa. Vyama vya wafanyakazi hutumiwa na wafanyakazi wenyewe kama chombo chao cha utetezi.
Wafanyakazi wanakuwa na matatizo kadhaa katika sehemu zao za kazi. Matatizo hayo hayatokani na amri ya Mungu. Hivyo wafanyakazi hawana budi kuyatatua ili kuondoa vikwazo katika shughuli zao za kazi na kuinua hali zao za maisha wakiwa wafanyakazi. Kwa mfano, katika kiwanda kuna mtaji, utawala/uongozi na nguvukazi. Kila kimoja kinajitegemea ingawa katika uendeshaji/ utendaji wa kazi vinategemeana na malengo yao pia yanatofautiana.
Mwekezaji ambaye ndiye wenye mtaji, lengo lake ni kupata faida kubwa kadri inavyowezekana ambapo utawala/uongozi upo pale kulinda na kukuza maslahi hayo na wafanyakazi huuza nguvu zao. Katika mazingira hayo, wafanyakazi huishia kunyonywa. Wafanyakazi kwa hivyo wanastahiki malipo ya haki na usawa kwa nguvukazi wanayoitoa. Uwezo wa mfanyakazi mmoja mmoja kupigania haki yake ni mdogo.
Hakuna
mafanikio ya maana anayoweza kupata mfanyakazi peke yake katika kupigania haki
yake. Ni kwa kupitia chama cha wafanyakazi pekee kinachounganisha pamoja nguvu
za wafanyakazi wote kinachoweza kuinua heshima ya wafanyakazi mbele ya waajiri,
na kupigania ujira utakaomwezesha mfanyakazi kuishi, kupata hali bora ya
maisha, na kupata marupurupu mengine.
Hayo
hasa ndiyo yaliyoleta haja ya wafanyakazi kujiunga pamoja na kuibuka na vyama
vya wafanyakazi. Kuunda vyama vya wafanyakazi ni haki ya msingi ya wafanyakazi
wenyewe. Jiunge na Chama cha Wafanyakazi sasa.