Zana za Kidigitali Kuchagiza Harakati za Vyama vya Wafanyakazi Tanzania

 

Katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia changamoto ya janga la ugonjwa wa Covid-19, elimu ya kidigitali imezidi kuwa muhimu. Ni katika kipindi hiki, vikao na mikutano kwa njia ya mtandao imeshamiri maeneo mbalimbali duniani. Hii inaonesha kuwa janga la Covid-19 limefungua ukurasa mwingine wa mawasiliano  baina ya mtu na mtu au taasisi na taasisi.

Baadhi ya washiriki kutoka vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia walioshiriki mafunzo ya TEHAMA yaliyoandaliwa na IndustriALL Global Union na FES- Tanzania. Yalifanyika jijini Dar es Salaam Novemba 24-26, 2020. Picha na Venance Majula - TUICO

Kwa kulitambua hilo, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), kilishiriki mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na IndustriALL Global Union wakishirikiana na Friedrich-Ebert-Stiftung (FES Tanzania) yaliyokuwa na lengo la kuvijengea uwezo Vyama vya Wafanyakazi na Asasi za Kiraia kwenye TEHAMA, matumizi ya mitandao ya kijamii na zana mbalimbali za kidigitali.

Akizungumza kwa njia ya mtandao katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Paule France Ndessomin, Katibu wa IndustriALL Global Union Kusini mwa Jangwa la Sahara alisema wakati wa janga la corona, vyama vya wafanyakazi duniani vimekuwa vikifanya kazi kwa njia ya mtandao.

“Tuna matumaini kuwa mafunzo haya yatawasaidia vyama vya wafanyakazi Tanzania, waweze kufanya kazi kwa njia ya mtandao, katika kusajili wanachama wapya na utekelezaji wa kampeni mbalimbali. Mambo yanabadilika sana.” alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa FES Tanzania Andreas Quasten alisisitiza umuhimu wa vyama vya wafanyakazi kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

“Mahitaji ya vyama vya wafanyakazi yanabadilika, hivyo ni muhimu kuyafumbata mabadiliko ya teknolojia. Ni lazima tutumie njia za kigitali ili tuendane na kasi ya mabadiliko hayo. Kama tunawahitaji vijana, basi tutumie teknolojia.” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TUICO, Sebastian Okiki, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA – TUICO, alisema  ni asilimia tatu tu ya  wafanyakazi wote nchini ndio wamejiunga na vyama vya wafanyakazi.

“Mafunzo haya yanakuja wakati sahihi kwani yatavisaida vyama kuwafikia wafanyakazi wengi na kwa urahisi. Kuna wafanyakazi wengi ambao hawako kwenye vyama vya wafanyakazi. Ni asilimia 3 tu ya wafanyakazi wote nchini ndio tunao kwenye vyama vya wafanyakazi.” alisema

Kwa upande wake, Raziah Mwawanga, Mkufunzi wa Mawasiliano, alikazia umuhimu wa vyama vya wafanyakazi kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya habari. Alisema wakati umefika kwa vyama vya wafanyakazi na Asasi za Kiraia kutumia redio, runinga na magazeti katika kuwafikia wanachama wake na wananchi kwa ujumla.

Carol Ndosi, Mkufunzi wa Elimu ya Kidigitali alisema kwa kipindi hiki cha janga la Covid-19, dunia imejifunza umuhimu wa elimu ya kidigitali katika kila nyanja ya maisha.

 “Kuna elimu ya msingi sana ambayo kila mfanyakazi anaihitaji katika kuboresha mawasiliano au kuongeza ufanisi wa kazi. Kutokana na janga la corona tumeona umuhimu wa wafanyakazi kujipatia ujuzi na maarifa ya kidigitali ili kuendelea kufanya kazi katika janga hili.” alisema

Inakadirikiwa kuwa Tanzania ina watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 14 ambao miongoni mwao, wapo wafanyakazi. Ni katika muktadha huu, teknolojia inakuwa miongoni mwa nyenzo muhimu kwa vyama vya wafanyakazi ili kuwafikia watu wengi  sambamba na utekelezaji wa mipango mbalimbali. Lakini uelewa wa mitandao ya kijamii, sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza matumizi yake unabaki kuwa kipaumbele.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika Novemba 24 hadi Novemba 26, 2020 jijini Dar es Salaam, yaligusia pia uelewa wa sheria na kanuni mbalimbali za mtandao, uandishi wa taarifa kuhusu vyama sambamba na namna ya kutangaza taasisi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Related

Youth 8324621316163301267

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress