Wajumbe wa KUT 2020-2025 Wakutana kwa Mara ya Kwanza

Mwenyekiti wa TUICO Taifa Ndugu Paul Sangeze, Januari 25, 2021 amefungua kikao cha kwanza cha Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) kilichofanyika mkoani Morogoro ambapo mbali na mambo mengine, Wajumbe wamejengewa uwezo kuhusu majukumu yao kwa ustawi wa chama.
Mkuu wa Idara ya Elimu TUICO Mwalimu Fredrick Mng'ong'o akiendesha semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TUICO Taifa kuhusu historia ya vyama vya wafanyakazi | Venance Majula/TUICO |
“Ndugu wajumbe, kikao hiki cha Kamati ya Utendaji ni kikao kikubwa cha kitaifa. Ninachowaomba, tunapokuwa kwenye vikao vyetu, michango yetu ielekezwe kitaifa, sio hoja za mikoani zinazohusu kiwanda kimoja au taasisi moja. Kila jambo liwe la kitaifa sio kila mmoja mmoja,” alisema Ndg. Sangeze.
Mwenyekiti wa TUICO Taifa Ndg. Paul Sangeze akifungua kikao cha Kamati ya Utendaji TUICO Taifa, Januari 25,2021, mkoani Morogoro | Venance Majula/TUICO |
Aidha, Ndg. Sangeze amewaasa Wajumbe wa KUT kushirikiana na viongozi wa TUICO kwenye ngazi za mikoa kuhakikisha chama kinapata wanachama wengi ambao ndio uhai wa chama chochote duniani.
“Ndugu Wajumbe niwaombe mshirikiane vizuri na viongozi wetu waliopo mikoani hususani inapotokea fursa ya kuingiza wanachama. Zikipatikana nafasi zitumieni vizuri kwa manufaa ya chama,” aliongeza Ndg. Sangeze.
Katibu Mkuu wa TUICO Ndg. Boniface Nkakatisi amesema hiki ni kikao muhimu kwa ajili ua utekelezaji wa shuguli za chama kwa mwaka 2021.
Katibu Mkuu wa TUICO Taifa Ndg. Boniface Nkakatisi akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji TUICO Taifa, Januari 25, 2021, Morogoro | Venance Majula/TUICO |
“Hiki ni kikao cha kwanza katika awamu yetu ya saba. Ni kikao ambacho tunachambua mambo mengi na kuyaweka vizuri kwa ajili ya rekodi zetu,” alisema Ndg. Nkakatisi.
Katika hatua nyingine, Wajumbe wamepatiwa historia fupi ya vyama vya wafanyakazi duniani. Fredrick Mng’ong’o, Mkuu wa Idara ya Elimu TUICO, alisema vyama vya wafanyakazi vilianza kwa lengo la kutetea na kulinda haki, heshima na masilahi ya wanachama na wafanyakazi kwa ujumla. Amesema “hiyo ndiyo kazi muhimu kwa chama chochote cha wafanyakazi. Na TUICO kama sehemu ya hivyo vyama, tumejidhatiti katika hilo,”
Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa TUICO Ndg. Tamim Salehe amewasilisha kuhusu kanuni, misingi na historia ya katiba ya TUICO na namna itakavyowaongezea ujasiri na maarifa katika utendaji wa majukumu yao. Wajumbe wa KUT wanatarajiwa kupitisha bajeti ya chama kwa mwaka 2021 ikiwa ni takribani mwezi mmoja umepita tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa TUICO mwezi Disemba 29, 2020.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe; Bi. Mwanaidi Bakari wa Mamlaka
ya Maji Lindi (LUWASA) na Ndg. Dismas Mgallah wa kiwanda cha nguo cha 21st Century Limited cha Mogororo, wamefurahishwa
na elimu kuhusu historia ya vyama vya wafanyakazi, katiba, kanuni na misingi ya
TUICO na wamesisitiza umoja ndani ya chama huku wakisema uwepo wa vijana ndani
ya KUT kunaashiria imani ya chama kwa vijana lakini maandalizi ya ushiriki wao
kwa kizazi hiki na kijacho.