Waziri Mhagama: Vyama vya Wafanyakazi ni Chachu ya Uboreshaji Mazingira ya Kazi

Waajiri nchini wametakiwa kutoogopa uwepo wa vyama vya wafanyakazi katika sehemu za kazi kwa kuwa ndio fursa kutatua changamoto zinazojitokeza mahala pa kazi.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu) Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, Desemba 29, 2020 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) uliofanyika mjini Morogoro.

Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (MB) akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa TUICO Taifa Desemba 29, 2020, Morogoro.

Waziri Mhagama alisema TUICO pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi nchini, vimekuwa tegemeo kwa wafanyakazi katika kulinda na kutetea haki, heshima na masilahi yao.

“Uwepo wa vyama vya wafanyakazi umekuwa ni nyenzo muhimu ambayo imeongeza tija na kujenga hali ya msukumo katika utendaji wa kazi wa wafanyakazi waliopo maeneo mbalimbali ya kazi nchini,” alisema Mhe. Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama alibainisha kuwa vyama vya wafanyakazi vimekuwa ni chachu ya uboreshwaji wa mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na uundwaji wa mabaraza ya kazi na ufungwaji wa mikataba ya hali bora kwenye maeneo ya kazi.

“Tumeshuhudia baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimekuwa chachu katika kuhamasisha majadiliano baina ya waajiri na wafanyakazi katika kufunga mikataba ya hali bora ya kazi ambayo imekuwa ikiwanufaisha wanachama,” alisema Mhe. Mhagama

Katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa TUICO Taifa, pamoja na kukitakia TUICO uchaguzi mkuu wa huru na haki, Waziri Mhagama alikipongeza Chama kutokana na uratibu mzuri wa shughuli zake.

Katika hatua nyingine,  Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Ndg. Tumaini Nyamuhokya pamoja na mambo mengine, aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutatua baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa kilio kwa wafanyakazi wengi akitolea mfano punguzo la kodi “Pay as You Earn” ambalo limewanufaisha wafanyakazi kwenye sekta binafsi na sekta ya umma.

Mwenyekiti wa TUICO Taifa, Ndg. Paul Sangeze alifafanua kuwa TUICO ni miongoni mwa vyama huru kumi na moja vya wafanyakazi nchini ambavyo vitaendelea kuboresha hali ya wanachama na wafanyakazi wakati wote wakiwa kazini.

“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na serikali pale tutakapoona kuna haja ya kutunga sheria sahihi za kazi na kuandaa sera nzuri za kuendeleza uchumi na manufaa kwa wafanyakazi,” alisema Ndg. Sangeze

Risala ya TUICO kwa Waziri Mhagama ilibainisha baadhi ya changamoto zinajitokeza katika utekelezaji wa shughuli za chama hicho na kuitaka serikali izifanyie kazi;- 

Mosi, kifungu cha 9(6) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6/2004 kuhusu “Senior Management Employee” ambao kwa mujibu wa kifungu hicho, Wafanyakazi hao wanaweza wasijiunge na vyama vya vafanyakazi. Baadhi ya waajiri, wamekuwa wakiwakataza hata wasimamizi (Supervisors), Makatibu Muhtasi, Watunza Vifaa (Store Keepers) kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa kigezo cha kuwa nao ni sehemu ya menejimenti.

Pili, ni kuhusu utatuzi wa migogoro. Kwamba Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) au Mahakama itakapoamuru mfanyakazi aliyeachishwa kazi kurudishwa kazini, mwajiri anaweza kuamua kumuachisha mfanyakazi kazi husika kwa kumlipa fidia kama inavyobainishwa katika kifungu cha 40(3) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6/2004. 

Tatu, ni kuhusu masharti ya usajili wa vyama vya wafanyakazi; yanaruhusu uwepo wa utitiri wa vyama, na vingine visivyo na malengo wala tija ya kusaidia wafanyakazi. Kigezo cha wafanyakazi ishirini kuwa na uwezo wa kuunda chama cha wafanyakazi kimetumiwa vibaya na baadhi ya waajiri na kuwa sehemu ya wao kujinufaisha wao kupitia mgongo wa wafanyakazi.

Changamoto nyingine ni kuhusu Ada ya Uwakala yaani “Agency Shop Fee” ambayo TUICO ilisema inaleta matatizo makubwa katika utekelezaji wa shughuli hasa matumizi yake. TUICO ilipendekeza kifungu hicho kisomeke kama ilivyokuwa kwenye sheria ya zamani yaani “Union Service Charge” kwa tafsiri ya Kiswahili “Ada ya Huduma” ambapo Katibu Mkuu wa chama atapokea ada zote na kuzipangia majukumu kwa manufaa ya chama na wanachama wake.

Walakini, TUICO iliiomba wizara  itafute ufumbuzi wa kero ya malipo ya kiinua mgongo kwa wastaafu, wenye mkataba wa muda maalumu na wanaopunguzwa kazi.

Naye, Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Bi. Pendo Berege alisema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa katiba na ndio sehemu pekee ya kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu chama. 

“Ofisi ya Msajili inategemea kuona vyama vya wafanyakazi nchini vinaendelea kutekeleza katiba za vyama vyao, kutambua mipaka ya kiutendaji na kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama,” alisema Bi. Berege

Mkutano huo Mkuu wa wa sita (6) wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) hufanyika mara moja katika miaka mitano na ni mkutano wa juu katika ufikiwaji wa maamuzi mbalimbali ya Chama.

Related

Recent News 7653742124474770889

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress