Siku ya Wanawake Duniani - 2021


Mwaka huu, kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani inayoangazia wanawake katika uongozi na namna ya kufikia baadaye yenye usawa, inasherehekea juhudi kubwa za wanawake na wasichana ulimwenguni kote katika kuandaa maisha ya siku zijazo.

Wanawake katika maeneo mbalimbali ya kazi duniani | Usanifu Venance Majula

Hata kama utandawazi umesababisha mamilioni ya wanawake wapate kazi za kulipwa, bado idadi yao katika kazi iko nyuma sana ukilinganisha na wanaume. Kukosekana kwa usawa wa kijinsia pia kumewaweka wanawake chini ya mlolongo wa thamani ulimwenguni - Katika kazi za malipo ya chini, kazi zenye mkataba mdogo, aina zisizo salama za kujiajiri, upatikanaji mdogo wa kazi bora na ulinzi wa kijamii. Ni wanawake ambao wana uwezekano mkubwa wa kukosa kazi kuliko wanaume.

Katika hatua nyingine, tofauti ya kijinsia ni kubwa kwenye maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania ambapo kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wa kike ni karibu mara mbili ya ile ya vijana wa kiume. Hii inaonesha, elimu pekee haiwezi kushinda vizuizi vya kimuundo katika masoko ya kazi.

Idadi ya watu kwenye nguvu kazi ulimwenguni kwa mgawanyo wa kijinsia| Usanifu Venance Majula


Ulimwenguni, wanawake hutengeneza senti 77 pekee kwa kila dola moja wanayopata wanaume. Hii ni sababu kuu ya kukosekana kwa usawa wa mapato kati ya mwanamke na mwanamme. Kwa viwango vya sasa, itachukua miaka 70 kuziba pengo hili. Sera za kazi ni jambo muhimu katika kuziba pengo hili. Bado wanawake wanakabiliwa na vizuizi zaidi katika kusawazisha kazi za kulipwa na majukumu ya familia. Sera na vizuizi mbalimbali, kama vile saa za kufanya kazi bila kubadilika na likizo uzazi, zinaweza kuzuia uhamaji wa wanawake kwenda nguvu kazi ya kudumu na kuwalazimisha kubaki kwenye ajira za muda.

Kwa upande mwingine, wanawake walio na watoto wako katika hatari zaidi ya kukosa usawa.  Kusini mwa Jangwa la Sahara, pengo la malipo ya kijinsia ni asilimia 31 kwa wanawake walio na watoto, ikilinganishwa na asilimia 4 kwa wanawake wasio na watoto. Aidha, ukatili dhidi ya wanawake ulimwengu wa kazi ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambao unaathiri wanawake bila kujali umri, eneo, kipato au hadhi yao katika kijamii.

Ombwe la malipo kwa wafanyakazi wanawake wenye watoto na wasio na watoto | Usanifu Venance Majula

Wanawake wanaweza kukumbana na unyanyasaji wa kingono wakiwa njiani kwenda, kutoka au wakiwa kazini kabisa. Kwa mfano asilimia 55 ya wanawake wamepata unyanyasaji wa kijinsia angalau mara moja tangu umri wa miaka 15. Kati ya hawa, asilimia 32 walikutana na hali hiyo mahali pa kazi. Ukatili dhidi ya wanawake unaweza kuzuia uwezo wa wanawake kiuchumi na kijamii na kuwa na athari kubwa kwa afya yao ya mwili na akili, ambayo inaweza kusababisha utoro au upotezaji wa kazi.

Hivyo, tunapowasherehekea wanawake, kwa pamoja tuangazie namna ambazo zitaleta msawazo wa kimasilahi kati yao na wanaume. Tutazame sera zetu zikoje? Zinatekelezeka? Ni rafiki? Wakati umefika kwa jamii kuondokana na mtazamo hasi kuhusu mwanamke. Mwanamke ni kiongozi, mwanamke sio chombo cha starehe, mwanamke ni mfanyakazi kama walivyo wengine. Mwanamke anastahili kuheshimiwa; ni mama na ni kioo cha jamii. Ni mzazi na mlezi. Tunawatakia heri ya siku hii muhimu ya kimataifa ya wanawake – Machi 08, 2021.

 

Related

Women 2890267013209140561

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress