TUICO YAFUNGA MKATABA WA HALI BORA NA SERENGETI


Leo Alhamisi, Aprili 08, 2021 Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimefunga Mkataba wa Hali Bora kati yake na Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL).

Hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam, imeshudiwa na Mwenyekiti wa TUICO Taifa Ndg. Paul Sangeze na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Dkt. Aggrey Mlimuka.

Naibu Katibu Mkuu TUICO, Ndg. Tamim Salehe (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries Limited Ndg. Mark Ocitti Ongom (kulia) wakibadilishana mikataba baada ya hafla ya utiaji saini mkataba wa hali bora kati ya TUICO na SBL | Aprili 08, 2021, Dar es Salaam

Katika hafla hiyo, Ndg. Sangeze aliwapongeza viongozi wa pande zote mbili kwa kufanikisha majadiliano ambayo yamepelekea utiaji saini wa makubaliano hayo huku akisisitiza kuendeleza ushirikiano thabiti kati ya Chama na Mwajiri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SBL Tanzania Ndg. Mark Ocitti Ongom alifurahishwa na mkataba huo ambapo alisema Serengeti Breweries Limited iko tayari kuusimamia ili kufikia tija, ufanisi kwa mwajiri na waajiriwa sambamba na utatuzi wa changamoto za wafanyakazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries Limited Ndg. Mark Ocitti Ongom akisaini mkataba wa hali bora kati ya TUICO na SBL | Aprili 08, 2021, Dar es Salaam


Katika hatua nyingine,
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka alizipongeza pande zote mbili (TUICO na SBL) kwa majadiliano hayo yenye tija huku akisisitiza kuwa sasa ni muda wa kutumia mkataba huo kuboresha masilahi ya mwajiri na wafanyakazi.

Dkt. Mlimuka amesema kutokana na utafiti walioufanya kwa vyama vya wafanyakazi nchini, TUICO ni Chama namba moja cha Wafanyakazi katika idadi na ubora wa Mikataba ya Hali Bora hali inayofanya TUICO kuendelea kuwa Chama imara.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa hali bora kati ya TUICO na SBL | Aprili 08, 2021, Dar es Salaam


Wakati huo huo, Ndg. Tamim Salehe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa TUICO na Msemaji Mkuu wa TUICO katika majadiliano hayo, amesema majadiliano hayo yalianza mwishoni mwa mwaka 2019 na kufikiwa mwezi Februari 2021 ambapo asilimia 75 ya mazungumzo hayo yamefanyika kwa njia ya mtandao (Zoom Meetings) kutokana na changamoto za Uviko-19. 

Pamoja na kuwashukuru wote waliofanikisha zoezi hilo, Ndg. Tamim aliwakabidhi Wakurugenzi Watendaji kutoka SBL na ATE, Mwenyekiti wa Majadiliano TUICO-SBL, Mkurugenzi Rasilimali watu SBL, zawadi za sare za Chama za Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi, 2021 na kuwakaribisha katika sherehe hizo zitakazofanyika kitaifa Jijini Mwanza.

 

Related

Recent News 8866491128866237571

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress