Rais Samia: Mishahara Itapanda Mwakani

 

Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza kwamba serikali imepunguza kodi ya mshahara hadi kufikia asilimia nane huku akiahidi kupandisha mishahara ya wafanyakazi mwakani baada ya ugonjwa wa Uviko-19 kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akizungumza na wafanyakazi katika maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika kitaifa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mei 01, 2021.

Katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza (Mei Mosi, 2021) Rais Samia amesema kodi ya mshahara (PAYE) inayotozwa kwenye mishahara ya wafanyakazi wa umma na binafsi imepunguzwa kutoka asilimia tisa ya awali hadi asilimia nane. 

Kwa mara ya mwisho serikali ilipunguza kiwango cha PAYE katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa na tangu hapo, miaka mitano sasa, haijawahi kubadilika. 

“Serikali imesikia ombi la wafanyakazi la kutaka kupunguziwa kodi inayotozwa kwenye mshahara (PAYE) na pia kutokukatwa kodi kwenye stahiki nyingine zisizokuwa za mshahara,” amesema Rais Samia 

Kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo la kodi litawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara unaozidi Shilingi 270,000 na usiozidi Shilingi 520,000.

Hata hivyo, wafanyakazi wanaolipwa mshahara angalau Shilingi 520,000 wanalazimika kulipa kodi ya ziada ukiondoa kodi ya msingi ya asilimia nane inayoongezeka kutokana na madara ya viwango vya mishahara. Mabadiliko hayo ya kodi yanatarajiwa kufanywa katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao, yaani 2021/2022.

Katika hatua nyingine, Mhe. Samia amesema mwaka huu hawezi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kutokana na kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za uchumi na athari zilizotokana na janga Uviko-19 (Covid-19).

“Nataka nitamke wazi mimi binafsi natamani kuona mishahara ya watumishi ingeongezwa. Ila kutokana na sababu mbalimbali, nimeshindwa kutimiza matamanio yenu kwa mwaka huu. 

“Kama mnavyofahamu kutokana na mlipuko wa Corona, kasi ya ukuaji wa uchumi duniani imeshuka. Kwetu Tanzania kasi ya ukuaji uchumi imepungua kutoka wastani wa asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7 mwaka huu,” ameongeza Rais Samia.

“Lakini niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa mwakani siku kama ya leo nitakuja na package (kifurushi) nzuri ya kupandisha mishahara,” ameongeza Rais Samia. 

Aidha, katika kuhakikisha anatekeleza ahadi hizo, Rais Samia ameagiza kuundwa kwa bodi ya mishahara itakayomwezesha kufahamu kiwango cha kuongeza katika mishahara ya watumishi wa umma na sekta binafsi.

Kwa miaka zaidi ya sita sasa, watumishi wa umma na sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia kutopandishiwa mishahara na kuwa na maslahi duni licha ya gharama za maisha kupanda kila siku.

Kuhusu wastaafu, Rais Samia amesema, ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu unamsikitisha na anatamani kuona kila mfanyakazi anayestaafu analipwa mara moja. Amesema serikali itaanza kulipa malimbikizo ya madai ya mafao ya wastaafu kuanzia Mei, 2021 huku akiwaagiza wakuu wote wa maeneo ya kazi kulipa madai yote kwa wakati na kutozalisha madai mapya.

Mapendekezo ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Wafanyakazi – TUCTA

Awali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, (TUCTA) kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Ndg. Said Wamba lilipendekeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi kuwa Shilingi 970,000 ili kumudu gharama za maisha.

Katibu Wamba alisema, mwaka 2006 walifanya utafiti na kubaini kuwa kima cha chini kilitakiwa kiwe Sh. 315,000 lakini Serikali haikutekeleza na mwaka 2014 walifanya utafiti mwingine na kubaini kuwa kima hicho kinatakiwa kuwa Sh. 720,000.

“Kwa sasa TUCTA tunapendekeza kiwango cha kumwezesha mtu kuishi kiwe ni Sh. 970,000. Hata hivyo wakati umefika kuwa na kiwango halisi kitaifa kinachomwezesha mtu kuishi yaani “living wage”, na kuweka malengo ya kufikia na kupunguza ugumu wa maisha,” alisema Katibu Wamba.

Alsema nyongeza hiyo inapaswa kufanyika mwaka 2021 kwa kuwa mishahara haijapanda kwa kipindi cha miaka sita kwa sekta ya umma na miaka minane kwa sekta binafsi huku gharama za maisha zikiendelea kupanda.

“Tunaiomba Serikali ipandishe mishahara ya wafanyakazi kwa sekta zote binafsi na umma mwaka huu,” alisisitiza Katibu Wamba.

Viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi wakiwemo Rais wa TUCTA Ndg. Tumaini Nyamhokya, Kaimu Katibu Mkuu TUCTA Ndg. Said Wamba, Mwenyekiti wa TUICO Ndg. Paul Sangeze (Mwenyekiti TUICO Taifa), Ndg. Boniface Nkakatisi (Katibu Mkuu TUICO Taifa) na viongozi wengine waandamizi wa TUICO wameshiriki maadhimisho hayo jijini Mwanza huku wakimhakikishia Mhe. Samia wanamuunga mkono na juhudi zake.

Related

Recent News 5693965189235860747

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress