LESCO YAASWA KUZINGATIA MISINGI YA MAJADILIANO YA UTATU

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameuasa uongozi wa Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO) kuzingatia mfumo wa majadiliano kwa kuzingatia utatu ili kuendelea kuleta tija kwa jamii inayoihudumia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kikao cha Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Dodoma tarehe 03 Novemba, 2021 Dodoma/Picha na OWM

Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza hilo kilichohusu uzinduzi rasmi wa baraza jipya na kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza linalotarajiwa kuhudumu kwa kwa miaka mitatu kwa mujibu wa sheria.Kikao kilifanyika mapema hii leo Novemba 3, 2021 Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alieleza ni lazima kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi kwa kuzingatia mchango wa baraza hilo katika masuala ya jamii, uchumi na ajira nchini. 

“Muundo wa Baraza unajumuisha wawakilishi wa Utatu na zaidi (Tripartite Plus) ambao ni Wajumbe wanaowakilisha maslahi ya Serikali, Waajiri, Wafanyakazi na Wajumbe wanaoteuliwa kwa kuzingatia utaalam wao,” alisema Waziri Mhagama.

Aliongezea kuwa, upo umuhimu wa kuzingatia misingi ya majadiliano ya utatu kwa ajili ya kuleta ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Baraza.

“Kimsingi, Muundo huu unakidhi matakwa ya Mkataba wa Shirika ka Kazi, ILO Na. 144 wa mwaka 1976 kuhusu Mashauriano ya Utatu (The Tripartite Consultation International Labour Standards) Convention No. 144 of 1976 ambao nchi yetu imeuridhia tarehe 30 Mei, 1983,”Alisisitiza Waziri Mhagama.

Waziri alilitaka baraza hilo kuhakikisha linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo la kumshauri Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na ajira kuhusu masuala ya Sera ya Soko la Ajira nchini, mapendekezo yeyote kutunga sheria kabla hayajawasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri, hatua za kuchukua kupunguza tatizo la ajira nchini na masuala yote ya ajira katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Mkuu wa Sekta ya Biashara kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) Wakili Peles Jonathan (wa kwanza kutoka kushoto) akishiriki Kikao cha Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO) kilichoanza leo Novemba 03, 2021 jijini Dodoma. Adv. Peles ni Mjumbe wa Baraza hilo/Picha na OWM

Aidha kuendelea kumshauri waziri kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi, kufuatilia na kushauri katika mabadiliko ya kisera ili kuendana na mabadiliko ya kidunia yanayotokea mara kwa mara.

Akitoa salamu wakati wa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Bi.Suzzane Ndomba alisema uwepo wa Baraza hilo utaleta majadiliano ya pamoja kama sheria inavyoeleza ili kukidhi malengo ya kuundwa kwake, na kuendelea kumshauri waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na ajira, nchini.

“Chama cha Waajiri nchini kitaendelea kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya baraza hili kwa kuzingatia sheria zilizopo kwa maslahi mapana ya nchi,”alisema Suzzane

Akitoa neno la shukrani  Mwenyekiti wa Baraza hilo Dkt. Samuel Nyantahe alimpongeza waziri kwa kuunga mkono jitihada za baraza hilo huku akiahidi kuendelea kuongoza baraza kwa ufanisi, weledi na kuzingatia utatu ili kuyafikia malengo ya uwepo wa baraza hilo.

“Tunashukuru kwa kuendelea kutuunga mkono tunaahidi tunayachukua maagizo yako kama yalivyo na tutayatekeleza ipasavyo, asante kutuongezea nguvu na tunaamini baraza litafanya kazi vizuri zaidi, tunaendelea kuahidi tutachapa kazi ambayo itakushangaza,”alisema Dkt. Nyahtahe

Related

Recent News 4996780811156947203

Post a Comment

emo-but-icon

TUICO CAMPAIGNS TO END GBV

ABOUT TUICO

TUICO on Twitter

TUICO ON FACEBOOK

Connect Us

item
Wordpress